Gatumba : mafuriko yalazimisha familia nyingi kukimbia
Makaazi mengi ya kata tisa za kijiji cha Gatumba tarafa ya Mutimbuzi (mkoa wa Bujumbura magharibi mwa Burundi) yalivamiwa na maji ya mto Rusizi (unaotenganisha Burundi na DRC) siku chache zilizopita. Viongozi tawala wanafahamisha kuwa idadi kamili ya walioathiriwa na mafuriko hayo itatangazwa ijumaa hii. HABARI SOS Médias Burundi
Wakaazi wanafahamisha kuwa madhara ni makubwa. Wandishi wetu walielekea katika eneo hilo. Wanasema ni hali ya kusikitisha ambapo ma mia ya watu wanalala nje usiku mzima pasina kuwa na vyoo.
” Tunalazimika kuacha makaazi yetu na kwenda kuishi karibu na barabara. Hatuna uwezo hata wa kwenda katika mashamba yetu. Yalivamiwa na maji. Nyumba zetu zilibomoka”, alibaini Arthemon Nishimwe.
Kwa mjibu wa Judith na hali ya kutia majonzi.
“Nyumba yangu imebomoka. Ni msamalia mwema anayeishi nje aliyenijengea nyumba hiyo. Kinachoniumiza sana moyoni ni kwamba walitukubalia kujenga ukuta kwa ajili ya kuzuia maji ya mto Rusizi yasivuke. Niliwaona hata raia kutoka China wakiwasili kufanya uchunguzi pamoja na viongozi wa Burundi “, alieleza mama huyo wa watoto wanne akiwa na majonzi. SOS Médias Burundi ilimukuta akiwasili kutafuta samaki wadogo maarufu ” Ndagala ” ambao anauzisha ili kuhudumia watoto wake.
Anaomba serikali kuingilia kati.
” Pesa iliyotengwa kwa ajili ya kujenga ukuta huo iliibiwa. Tunaomba rais wa Burundi kuingilia kati. Anatakiwa kujuwa namna wapiga kura wake wanavyosumbulika. Tunaelekea kufa na njaa hapa”, alisisitiza mama huyo ambaye anazidi kuwa hata wakiwapa chakula, hawatapa mahala ambapo wanaweza kuandalia chakula hicho”.
Kwa mjibu wa Juma Rukundo mwenye umri wa miaka zaidi ya sitini, ” tunahitaji angalau nyasi kwa ajili ya kuezeka tu jumba twetu”.
Lucie Gahimbare ni kiongozi maarufu nyumba kumi, alilazimika kwenda na watoto wake kwa hofu ya kuuwawa na mafuriko. Analaani hali hiyo inayorejea kila mara katika msimu wa mvua.
” Hata watoto wamezoea hali hiyo . Hii ni mara ya tatu mfururizo kila mwaka. Wakati wa mafuriko tunalazimika kuyahama makaazi yetu na kutafuta hifadhi barabarani” alilalamika mama huyo anayetegemea msaada kutoka serikalini haraka iwezekanavyo.
” Bora nisijieleze kuhusiana na hali hiyo. Imekuwa mara ya tatu mfururizo tukikabiliwa na hali hii na jibu : serikali inakwenda kuchukuwa hatua dhidi ya tatizo hili. Mara nyingi tunajiuliza iwapo sisi ni warundi. Hakika tulitupiliwa. Mungu mwenyewe atatusaidia”, alilaani baba mmoja.
Familia nyingi zililazimika kukimbia makaazi yao, vyanzo eneo hilo viliarifu.
Mkuu wa tarafa ya Mutimbuzi Siméon Butoyi alifahamisha kuwa sensa bado kumalizika.
” Wakaazi wa kijiji chote cha Kinyinya walitoroka. Wanapokelewa katika vituo vilivyoandalia kupokea waathiriwa hao” alifahamisha na kuzidi kuwa idadi ya walioathiria na mafuriko hayo itajulikana ijumaa hii.
Idara ya kushughulikia majanga iliahidi kuwa suluhu litapatikana mnamo siku zijazo.
” Serikali inahitaji milioni 20 dola za kimarekani kwa ajili ya kujenga ukuta kwenye mwambao ili kuzuia mto Rusizi kuvuka na kusababisha madhara”, alifahamisha brigedia jemedali Anicet Nibaruta kiongozi wa kitengo hicho.
Na kutahadharisha kuwa ” wakaazi wa maeneo ya Mushasha 1 na Mushasha 2 wanatakiwa kuhamishwa mara moja na kupewa makaazi mapya katika mikoa ya Bujumbura na Rumonge ( kusini- magharibi)”.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, angalau watu 10 walipotea, karibu wengine elfu 40 walilazimika kupewa hifadhi katika vituo kwa ajili ya wakimbizi wa ndani kutokana na mafuriko hayo katika kijiji cha Gatumba. Angalau wakaazi elfu saba walihamishwa makaazi yao yalikuwa katika maeneo hatari zaidi kulingana na ripoti ya serikali ya Burundi.
Mwaka huu hadi mwezi mei, eneo la Imbo ambako kunapatikana kijiji cha Gatumba pamoja pia na eneo la Mirwa, kutapatikana mvua nyingi kwa mjibu wa idara ya kitaifa ya tabia nchi.