Ngozi : mfuasi wa chama cha CNL apatikana akiwa maiti

Ngozi : mfuasi wa chama cha CNL apatikana akiwa maiti

Muili wa Gilbert Ndacayisaba mwenye umri wa miaka 47 ulipatikana katika shamba la miti ya mikaratusi alhamisi mchana. Mkaazi huyo wa kijiji cha Karungura tarafani Mwumba mkoa wa Ngozi (Kaskazini mwa Burundi), alikuwa mmoja kati ya viongozi wa chama hicho cha upinzani katika eneo hilo. Watu wake wa karibu wanadai kuwa huenda aliuwawa na Imbonerakure (wajumbe wa tawi la vijana wa chama cha CNDD-FDD). Wawili kati ya Imbonerakure wanne wanaotuhumiwa mauwaji hayo walikamatwa. HABARI SOS Médias Burundi

Muili wake ulikuwa ndani ya mfuko wakati ulipogunduliwa na watoto waliokuwa wakitafuta kuuni za kupikia.

” Tuliona mfuko ambao ndani yake kulikuwa kitu. Tuliangalia na tukagundua kuwa ndani kuna maiti. Tulipata woga, tukatoa taarifa kwa wakaazi”, alieleza shahidi mmoja katika wale waliofanya ugunduzi huo wa kutisha.

Kwa mjibu wa mfuasi wa chama cha CNL katika kijiji hicho cha Karungura, marehemu alikuwa miongoni mwa viongozi wa chama hicho cha upinzani eneo hilo. Huenda aliuwawa kutokana na msimamo wake wa kisiasa.

” Mara nyingi alifanyiwa vitisho na Imbonerakure wa kijiji cha Karungura ambao nia yao walitaka ajiunge na chama tawala cha CNDD-FDD lakini bila kufanikiwa. Waliahidi hata kumupa adhabu. Hatukuamini kuwa wangefikia hata kumumalizia maisha”, walieleza wafuasi wa chama hicho.

Imbonerakure wawili walikamatwa, wawili wengine walikimbia. Wanatuhumiwa kuhusika na mauwaji hayo.

Waliokamatwa, wanazuiliwa katika kamishena ya polisi ya Mwumba.

Polisi inahakikisha kuwa uchunguzi unafanyika.

Gilbert Ndacayisaba alitoweka jumatano tarehe 6 aprili jioni wakati akielekea nyumbani kwake kwa mjibu wa watu wa karibu yake. Wanaomba ufanyike uchunguzi huru.

Previous DRC : sheria kuhusu uhuru wa vyombo vya habari inataraji kutangazwa
Next Ituri: watoto waangamia katika mashambulizi ya makundi ya silaha mkoani Ituri