RDC (Ituri) : angalau wananchi 40 waliuwawa na waasi wa CODECO

RDC (Ituri) : angalau wananchi 40 waliuwawa na waasi wa CODECO

Vijiji vitatu vya eneo la Banyali Kilo, wilayani Djugu katika mkoa wa Ituri mashariki mwa DRC vililengwa na mashambulizi ya wakati mmoja ya waasi wa CODECO (shirikisho kwa ajili ya maendeleo ya Kongo) asubuhi ya ijumaa tarehe 14 aprili. Matokeo yake ni wananchi wa kawaida 37 kuuwawa, maduka kuporwa na nyumba kuchomwa moto kwa mjibu wa kiongozi wa mashirika ya kiraia ya eneo hilo. Kijiji cha Matete pia kililengwa na kundi hilo. Watu nane waliuwawa. HABARI SOS Médias Burundi

Kulingana na kiongozi wa mashirika ya kiraia eneo hilo, shambulio la kwanza lililenga vijiji vya Kilo na Itendei .

” Zaidi ya wananchi 37 waliuwawa kikatili kwa kukatwa vichwa na waasi wa CODECO kwa kutumia mapanga. Miili yao ilikusanywa kwenye kituo cha kibiashara cha Kilo”, aliripoti Jean Basilok mwakilishi wa mashirika ya kiraia eneo hilo.

Shambulio jingine lilifanyika katika kijiji cha Matete kwenye umbali wa kilometa 4 kutoka tarafa ya vijijini ya Mungbwalu. Kulingana na vyanzo eneo hilo watu 8 waliuwawa.

Taarifa hizo zimethibitishwa na msemaji wa jeshi la jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo wilayani Ituri.

Luteni Jules Ngongo alihakikisha kuwa ” wanajeshi wa FARDC wanawafuatilia waasi “.

Idadi kubwa ya wananchi waliouwawa ni wajumbe wa jamii ya Nande ambao wanaendesha biashara na kilimo eneo hilo.

” Waliuwa wananchi wa kawaida na kupora maduka. Makaazi ya watu pia yaliporwa na badaye kuchomwa moto “, wanalaani wakaazi.

Ifahamike kuwa shambulio hilo lilivuruga shughuli zote katika tarafa ya kijijini ya Mungbwalu iliyoshuhudia milio ya silaha mchana wote wa ijumaa.

Gratien Iracan mbunge wa kitaifa anasema kuwa ni watu 62 waliouwawa. Anatoa wito kwa serikali ” kuimarisha ulinzi ” katika eneo hilo”.

Ituri pamoja na mkoa wa kivu kaskazini mikoa hiyo miwili inayopakana ya mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati inaendelea kutumbukia katika usalama mdogo licha ya rais Tshisekedi kuanzisha utawala wa kijeshi tangu mei 2021 katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini na kuwepo kwa kikosi cha kikanda cha EAC na kikosi kinachokosolewa cha Monusco (ujumbe wa umoja wa mataifa nchini DRC).

Previous Bujumbura : kongamano lisilokuwa la kawaida la chama cha CNL lasimamishwa kwa kosa "la tahajia"
Next Masisi: mapigano makali kati ya kikosi cha Burundi na kundi la M23