Burundi : bei ya mafuta ya gari yapanda kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili

Burundi : bei ya mafuta ya gari yapanda kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili

Bei ya mafuta ya gari aina ya petroli (essence) ilitoka kwenye bei ya 3895 na kupanda hadi 4550 sarafu za Burundi sawa na ongezeko la franka 665. Bei ya mazout iliyokuwa 3795 sarafu za Burundi sasa ni 4250 sawa na ongezeko la 455. Hatua hiyo ilitangazwa na waziri wa nishati Ibrahim Uwizeye jumatatu jioni. Alisema kuwa hali hiyo imesababishwa na msimamo wa uchumi wa kimataifa. HABARI SOS Medias Burundi

Hatua hiyo ilitangazwa katika mkutano na wandishi wa habari uliofanyika katika mji mkuu wa kibiashara wa Bujumbura. Waziri Ibrahim Uwizeye alieleza kuwa hali hiyo ya kupandisha bei ya mafuta ya gari imesababishwa na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kwenye soko la kimataifa”.

Bwana Uwezeye alitangaza kuwa wizara anayoiongoza inashuhudia kwa kipindi fulani changamoto katika uagijazi wa mafuta kutoka soko la kimataifa, kanda na taifa kutokana na hali ya uchumi wa dunia.

” Mafuta ya gari sio bidhaa inayozalishwa nchini, na bei yake inapangwa kwa ngazi ya kimataifa. Burundi inaathirika na mabadiliko ya bei kwenye soko la kimataifa”, alieleza.

Juhudi kubwa

Kulingana na waziri, viongozi wa Burundi walifanya kila linalowezekano ili kuepusha bei kupanda kwa kiwango kikubwa.

” Serikali ilisamehe ushuru ili kuepusha bei ya mafuta ya gari kupanda kwa kiwango kikubwa. Isingekuwa hivyo kwa mfano mazout imepatikana kwa bei kubwa tusingefanya juhudi kubwa”, alisisitiza waziri na kusema ni hatua inayozingatia maslahi ya wananchi wa Burundi”.

Safari zisizokuwa za lazima na kubadili mwendendo

” Ni budi kujiepusha na safari zisizokuwa za lazima, na kama una gari nne nyumbani, basi egesha tatu au ukaziuzishe na kubaki na moja peke. Ni lazima tukubali hali hii ambayo ni ya kimataifa “, alishahuri Ibrahim Uwizeye.

Na kuendelea : ” Ni lazima tubadili mwenendo. Kuna familia ambapo baba anaendesha gari lake, kadhalika mama na mtoto. Wangetumia gari moja ili kwenda kazini. Na kama haiwezekani, chukuweni basi na mutakapowasili kwenye kituo cha basi mjini kati , tembea na miguu hadi kazini “.

Waziri huyo aliendelea kusema kuwa licha ya juhudi zilizofanywa, serikali ililazimika kupandisha bei ili kuhakikisha taasisi zinaendelea kufanya kazi, na usafiri wa watu wa vitu unaendelea”.

Kuvunjika moyo

Katika mji wa kibiashara wa Bujumbura, wakaazi wengi wanasema kuwa ” bei ya bidhaa zingine mahitajio muhimu na nauli itapanda “.

” Serikali ingetakiwa kutuhurumia . Zingatieni kuwa bei ya mafuta ya gari imepanda katika kipindi cha chini ya miezi miwili kwa wananchi ambao wanakabiliwa na umasikini. Maisha hatawezekana tena. Tutapata matatizo ya usafiri, kulisha watoto wetu na kuhudumia familia zetu. Athari za kupanda kwa bei ya mafuta ya gari, zitashuhudiwa katika maisha yetu ya kila siku hata katika kodi ya nyumba. Kwanza kabisa kusafiri kutoka Bujumbura na kuelekea mikoani ni kama kwenda nchini Kenya “, wanalaani wakaazi wa mjini na kuomba serikali kubadili hatua hiyo.

Kulingana na wanaofanya kazi ya usafiri na wamiliki wa gari za uchukuzi wa umma, serikali inatakiwa kupanga upya bei ya nauli”.

Mara ya mwisho kwa bei ya mafuta ya gari kupanda ilikuwa mwezi julai iliyopita, baada ya kipindi kirefu cha uhaba wa bidhaa hiyo inayochukuliwa na wataalam kama msingi wa uchumi wa nchi na ambayo bado ni adimu kwenye masoko.

Nchi hii ndogo ya Afrika mashariki inashuhudia uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo ya mafuta. Wananchi wanadai kuwa ” walitupiliwa “.

Watalaamu wa ndani walitoa wito kwa viongozi wa Burundi kuitisha mkutano mkuu wa wadau wa sekta ya mafuta ili kutafuta suluhu la kudumu kwa uhaba wa mafuta ya gari wa zaidi ya miezi kumi na nane.

” Ni tatizo linaloendelea. Tumekuwa kicheko. Wananchi wa Burundi wanatakiwa kuona mafuta ya gari hapa na katika ghala zetu mjini Dar Es Salam. Hata Kongo ambayo inakabiliwa na mzozo na ambayo tunasaidia katika maswala ya usalama haina matatizo ya kuagiza mafuta ya gari kutoka nje “, alibaini mwezi julai Faustin Ndikumana kiongozi wa shirika la PARCEM linalodai kutetea utawala bora.

Kwa mujibu wa Noël Nkurunziza katibu mkuu wa shirika la wanunuzi (ABUCO), ” ni maskitiko kuona bei zikipandishwa pasina kumushirikisha mnunuzi wa Burundi”.

” Ukiangalia uwezo wa kununua wa raia wa Burundi kwa sasa, na kupanda kwa bei, haiwezekani kumudu gharama za maisha”, alilaani.

Maoni ya viongozi

Kwa mara kadhaa, rais Evariste Ndayishimiye na viongozi wengine wakuu akiwemo spika wa baraza la bunge Daniel Gélase Ndabirabe walihakikisha kuwa ” Burundi ni kama pepo”, wakidai kuwa wananchi wa nchi jirani wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa vyakula na bei kupanda kwa kiwango cha juu kiasi kwamba wanakuja kwenye soko la bidhaa nchini Burundi na kuzichukuwa zote sababu bei ni ya kawaida.

Wawili hao kwa kipindi tofauti, walitangaza kuwa ” Burundi haina haja ya pesa za kigeni ( dola za kimarekani ) wananchi wa Burundi wanatumia sarafu ya Burundi ili kununua kile wanachohitaji kwenye soko la ndani “.

Previous Gitega : hakuna sheria miaka 27 baada ya mauwaji ya askofu Joachim Ruhuna
Next DRC (Uvira) wakimbizi wawili wenye asili ya Burundi wakamatwa kwa jaribio la mauwaji