Nduta (Tanzania) : uhaba mkubwa wa damu wakati wa mripuko wa malaria

Nduta (Tanzania) : uhaba mkubwa wa damu wakati wa mripuko wa malaria

Damu zimekosekana katika vituo vya afya ndani ya kambi ya Nduta nchini Tanzania. Sababu kuu ya hali hiyo ni watoa damu kuacha kutoa damu kutokana na ukosefu wa chakula kuzuri. Vituo vya afya vinapata wasi wasi huku mripuko wa maradhi ya malaria ikiacha madhara. HABARI SOS Médias Burundi

Katika hospitali na vituo vya afya takriban vyote katika kambi ya Nduta nchini Tanzania, kupata damu ni mtihani mgumu. Wanaoathiriwa pakubwa na hali hiyo ni akinamama wajawazito, watoto wa chini ya miaka mitano na wagonjwa waliofanyiwa upasuaji kama akinama waliopasuliwa ili kijifungua.

Uhaba huo wa damu unaanza kusababisha vifo.

” Mtoto alifariki kutokana na kukosa damu. Alikuwa na ugonjwa wa malaria kali iliyosababisha damu kukosekana. Tunashuhudia wasi wasi mkubwa katika idara zote”, alieleza muhudumu mmoja wa kujitolea katika matibabu.

Sababu kuu ya hali hiyo ni kutokana na mazingira mabaya ya chakula kwa wakimbizi ambao wanakataa kutoa damu.

” Chakula kilipunguzwa sana mara tatu tangu mwanzo wa mwaka huu na kila mwanzo wa mwezi, tunajiandaa kwa punguzo jingine. Kwa hiyo, vipi tunaweza kutoa damu wakati ambapo hakuna cha kurudisha damu ! Kinyume cha hapo, mtu anayetoa damu atapata maradhi na yeye pia atahitaji kupewa damu. Hakika hali hiyo ni ya ajabu “, wakimbizi wa Burundi katika kambi ya Nduta wanalaani.

Viongozi wa kiafya walianzisha kampeni isiyokuwa ya kawaida kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.

” Kampeni ya kukusanya damu inafanyika kwa sasa kila baada ya wiki mbili ili kujaribu kupata angalau mifuko michache ya damu. Lakini tunashuhudia kuwa watu hawaitiki kwa wingi kama ilivyokuwa kabla. Tunaweza kupata kwa tabu watu takriban kumi katika kipindi hichi chote”, vinahakikisha vyanzo vyetu katika vituo vya afya, na kukumbusha kuwa aina hiyo ya kampeni ilikuwa ikiandalida kila baada ya miezi mitatu.

Wauguzi wanaeleza kuwa katika kipindi cha kawaida, hospitali ilikuwa na uwezo wa kugawa damu kwenye vituo vya afya vya Tanzania vya karibu lakini wanafahamisha kuwa kwa sasa ” hata kambi haijitoshelezi na hifadhi yake haina damu”.

Ukosefu huo wa damu unawatia hofu wahudumu wa afya na wakimbizi ikizingatiwa kuwa uhaba huo umetokea wakati wa mzozo wa ugonjwa wa malaria.

” Tunawapokea wagonjwa wengi wanaohitaji kupewa damu. Na wakati wanapokuwa na dharura kubwa , kwa mfano akinamama wanaotakiwa kijifungua kwa upasuaji, tulikuwa tukiwapeleka kwenye hospitali ya viwango nje ya kambi huku wakiingiziwa damu. Ghala yetu ikiwa tupu, inamaanisha kuwa tuna tatizo kubwa la kiafya” wanasema wahudumu wa afya ndani ya kambi.

Shirika la waganga wasiokuwa na mipaka ( MSF) lilitoa ushirikiano kwa IRC ( international Rescue Committee) katika kampeni ya kutibu ugonjwa wa malaria ili kujaribu kukabiliana na mripuko huo.

” MSF inaweka nguvu zake katika vituo vya afya. Juhudi za pamoja ni za aina tatu : vipimo kwa ugonjwa huo, usambazaji wa vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa na kupuliza madawa katika majumba”, wanaeleza wahudumu wa afya wanaojitolea.

Zoezi hilo linafanyika ndani ya kambi na katika vijiji vya karibu ili kujaribu kupunguza madhara katika kambi ya Nduta, eneo hatari sana linapokuja swala la mzozo huo wa afya kama huo.

Kambi ya Nduta inawapa hifadhi wakimbizi kutoka Burundi zaidi ya 76.000

Previous Kirundo : mvulana mmoja alifariki dunia baada ya kupigwa na Imbonerakure
Next Mabayi : waziri mkuu wa serikali ya Burundi atishia kuwauwa watu wote wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda waliopiga kambi ndani ya msitu wa Kibira