Mabayi : waziri mkuu wa serikali ya Burundi atishia kuwauwa watu wote wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda waliopiga kambi ndani ya msitu wa Kibira

Mabayi : waziri mkuu wa serikali ya Burundi atishia kuwauwa watu wote wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda waliopiga kambi ndani ya msitu wa Kibira

Tangazo lilitolewa jumanne hii kando na mkutano wa waziri mkuu Gervais Ndirakobuca na wawakilishi wa viongozi, maafisa wa usalama pamoja na waakazi wa tarafa ya Mabayi mkoa wa Cibitoke (kaskazini magharibi mwa Burundi). Alizidi kusema kuwa viongozi wa Burundi watafanya sensa kwa ajili ya kuwafukuza kwao raia wa Rwanda wanaoishi tarafani Mabayi. Hivi karibuni, kiongozi wa Imbonerakure (wajumbe wa tawi la vijana wafuasi wa chama cha CNDD-FDD) tarafani aliuwawa na waasi wa Rwanda waliopiga kambi katika msitu wa hifadhi wa Kibira. Mkuu wa tarafa, viongozi wengine wawili, pamoja na Imbonerakure watatu walisimamishwa. Walituhumiwa kushirikiana na waasi. HABARI SOS Médias Burundi

Jumanne hii, Gervais Ndirakobuca mjumbe wa zamani wa kikundi cha waasi wa kihutu na mzaliwa wa tarafa ya jirani ya Bukinanyana alikuwa na hasira nyingi. Kwa mjibu wake, wananchi wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda wanajiweka katika hatari kubwa, madhara na matatizo ambayo hawawezi kufikiria.

” Mnacheza na moto”, alisisitiza.

Mpango wa kuwauwa wote wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda

Gervais Ndirakobuca alikwenda moja kwa moja. Wananchi wote wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda waliopiga kambi ndani ya msitu wa hifadhi wa Kibira wanajikokotea radu za viongozi wa Burundi.

” Kuna hatari ya kuzika angalau watu 300 kwa mpigo. Hatutakubali wanajeshi wetu kuendelea kuuwawa kila wakati. Kwa nini mnawasaidia hao watu ? Kama wako na malalamiko, waende kutafuta huduma ndani ya nchi yao. Wanaweza kusababisha matatizo mengine ambayo hamuwezi kufikiria”, alitangaza kwa sauti ya kusisitiza.

Na kuendelea kusema, ” Acheni kushirikiana na watu hao kabla hamjachelewa “.

Uwezekano wa kuitenga tarafa ya Mabayi

Kwa mujibu wa Bwana Ndirakobuca, hali inayojira tarafani Mabayi, haileti faida kwa tarafa hiyo au kwa mkoa wa Cibitoke, mbali zaidi kwa nchi ya Burundi.

” Mnataka tuwe tunawazika watu kila siku kama ilivyokuwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ? Mnataka watu walale katika vichaka na kung’atwa na mbu, kuwaweza katika hatari kupatwa na maradhi ya kila aina? Hayo ndio mnataka kurejesha hapa Mabayi ? Hii ni ilani ya mwisho “, alitahadharisha Gervais Ndirakobuca.

Na kuendelea” amani haina bei. Iwapo kesho tutafunga barabara kwa lori zote zinazopita hapa kutoka Ngozi ( kaskazini) zikibebea unga , tukifunga upande wa tarafa ya Rugombo ( daima katika mkoa wa Cibitoke) na kuzuia kuja hapa kwa magari yanayobebea vyakula, mutaathirika. Mutapata matatizo lakini bahati mbaya hii ndio hatua itakayofuata. Hatuna chaguo jingine “.

Sensa ya watu wa asili ya Rwanda kwa ajili ya kuwafukuza

Waziri mkuu wa serikali ya Burundi alitangaza pia ” sensa kufanyika kwa ajili ya kuhesabu wananchi wote wa Rwanda wanaoishi tarafani Mabayi kwa ajili ya kuwarudisha nchini Rwanda “.

Viongozi tawala wala rushwa kuwekwa jela

Muasi huyo wa zamani wa kihutu alikuwa wazi kabisa katika maneno yake. Viongozi wa nchi hiyo ndogo ya Afrika mashariki hawataki kusikia tena viongozi wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda au wanaowapa huduma.

” Leo, nimewatolea wito nyinyi wananchi sababu nataka ukweli wote ujulikane. Wawakilishi wetu katika vijiji na maeneo mengine , hao waliouzisha roho yao kwa shetani, tafadhari, semeni utambulisho wao wote hapa. Kama mnaogopa, njooni kuniambia kwa siri. Wote tutawatuma jela […] na tutawachilia huru baada ya amani kurejea “, alisisitiza.

Anawataja hao wanaoshirikiana na waasi wa Rwanda kama ” funza ndani ya nguo zetu”, na kuongeza kuwa haikubaliki kuendelea nao.

Kulingana na Gervais Ndirakobuca, hakuna amani tarafani Mabayi.

Katika usiku wa tarehe 9 agosti iliyopita, Isidore Niyongabo maarufu kama Maisha mkuu wa Imbonerakure tarafani aliuwawa na waasi wa Rwanda wa kundi la silaha la FLN kulingana na vyanzo vyetu. Wakati huo huo, mkuu wa tarafa ya Mabayi Nicodème Ndahabonyimana, viongozi tawala wengine wawili eneo hilo pamoja na Imbonerakure watatu walikamatwa. Wanazuiliwa katika gereza la SNR ( idara ya ujasusi) ndani ya mji mkuu wa kibiashara wa Bujumbura. Wanatuhumiwa kushirikiana na waasi.

Wakinufaika na ushirikiano na baadhi ya maafisa wakuu katika jeshi , na viongozi tawala ambao wanapewa dhahabu inayochimbwa kinyume cha sheria katika msitu wa Kibira, waasi hao waliopiga kambi ndani ya msitu huo mkubwa wamekuwa wakipoteza uungwaji mkono kutokana na kufufuka kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kigali na Gitega kwa mjibu wa vyanzo katika taasisi ya usalama.

Hivi karibuni, angalau sita kati yao waliuwawa katika mapigano na jeshi la FDNB ( jeshi la Burundi) , wengine wengi walijeruhiwa na kukamatwa . Wanazuiliwa na kupata matibabu ndani ya mji mkuu wa kiuchumi. Katika miaka michache iliyopita, wafanyabiashara wengi, viongozi eneo hilo pamoja na wajumbe wa tawi la Imbonerakure walikamatwa na kupelekwa jela kwa kosa la kushirikiana na waasi hao. Idadi kubwa wanazuiliwa katika gereza kuu ya Bujumbura maarufu Mpimba.

” Viongozi wa Burundi wanatakiwa kuachana na tahadhari hizo na hivyo kuanza vitendo ” alidai mwandishi wa habari mmoja anayefahamu kuhusu faili hiyo.

Previous Nduta (Tanzania) : uhaba mkubwa wa damu wakati wa mripuko wa malaria
Next Bururi : kiongozi wa gereza kuu ya Murembwe na wafanyakazi wenzake wawili wapewa adhabu ya kifungo cha miaka 7 na miezi 6 jela