Burundi: utawala wa rais Ndayishimiye unafanya mauwaji kama ule wa mtangulizi wake Nkurunziza

Burundi: utawala wa rais Ndayishimiye unafanya mauwaji kama ule wa mtangulizi wake Nkurunziza

Shirika la kutetea haki za binadamu la Iteka linatoa tahadhari . Katika ripoti yake ya mwisho, shirika hilo la zamani kabisa la kutetea haki za binadamu nchini Burundi limetoa orodha ya watu 4040 waliouwawa tangu aprili 2015 hadi aprili 2023. Shirika la Iteka linakwenda moja kwa moja. Kwa mjibu wake, takwimu hizo zilipatikana katika utawala wa watu wawili ambao walikabidhiwa uongozi wa nchi ya Burundi na kuonyesha matokeo yanayofanana kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na usalama. HABARI SOS Médias Burundi

Kulingana na shirika la Iteka, tangu kuanza kwa mgogoro wa kisiasa nchini Burundi kuanzia mwaka wa 2015 kutokana na nia ya hayati rais Pierre Nkurunziza ya kugombea muhula ya tatu ” kinyume cha sheria na katiba “, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliripotiwa hususan mauwaji, watu kukamatwa na kufungwa kinyume cha sheria, wengine kupotea , unyanyasaji wa kinjisia pamoja na visa vya mateso hadi uchaguzi wa rais mpya Evariste Ndayishimiye.

” Chini ya utawala wa Pierre Nkurunziza aprili 2015 hadi 2020, shirika la Iteka liliorodhesha watu 2.292 waliouwawa, maiti 626 ziligunduliwa, watu 564 walitekwa nyara au kupotea mara moja, 1.027 walifanyiwa mateso, wengine 11.152 walisimamishwa kinyume cha sheria pamoja na watu 263 wahanga wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia. Maelezo hayo yanatolewa katika ripoti shirika hilo ambalo liko uhamishoni.

Shirika hilo la Iteka linasema kuwa tangu alipofika kwenye utawala mwezi juni 2020, rais Ndayishimiye alionekana akitoa hutba nzuri na kuahidi kuimarisha usalama, haki za binadamu na utawala bora nchini Burundi. Ujumbe huo ulileta matumaini kwa wananchi wa Burundi na jamii ya kimataifa.

Hata hivyo shirika hilo linalaani kuwa hakuna vitendo vilivyofuata ujumbe huo.

” Shirika la Iteka liliweza kuorodhesha watu 1.748 waliouwawa, maiti 755 kupatikana, 133 walitekwa, 198 walifanyiwa mateso, 1920 wengine walikamatwa kinyume cha sheria pamoja na 348 waathiriwa wa unyanyasaji wa kinjisia. Katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake, imeshuhudiwa kuwa hutba zake nzuri zinaishia kwenye matangazo” linaarifu shirika hilo ambalo hunukuliwa na taasisi za marekani kama kielelezo katika maswala ya haki za binadamu nchini Burundi.

Shirika hilo linadai kuwa hamna mabadiliko katika uwanja wa usalama na haki za binadamu ambapo watu 4040 waliathiriwa wakati wa utawala wa watu hao wawili.

” Iwapo utawala wa rais Evariste Ndayishimiye hautaongeza nguvu katika kudhibiti uhalifu ulioshuhudiwa katika miezi hii 34 ya utawala wake, kuna hatari utawala wake ukawa wa mauwaji zaidi licha ya hali inayofanana kama amani”, anatahadharisha Anschaire Nikoyagize kiongozi wa shirika la Iteka.

Lakini mashirika ya ndani ya nchi yanasema ” ni ripoti isiyokuwa sahihi ambapo na takwimu zake si sahihi “.

” Shirika la Iteka lilivimbisha hesabu. Takwimu tulizonazo ziko chini na mbali sana na hizo zilizotangazwa na shirika la Iteka. Katika maswala ya kutetea haki za binadamu, sio sahihi kuchukuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na ajali au waliouwawa kufuatia mizozo ya familia na kuzijumulisha na zile za watu waliomaliziwa maisha “, anathibitisha Gérard Hakizimana kiongozi wa shirika la Folucon-F linalopiga vita upendeleo. Hata hivyo, hakuweka wazi takwimu linazotolewa na shirika analoliongoza kuhusu mauwaji na utekaji.

Lakini Bwana Hakizimana alifanikiwa kutoa idadi ya wafanyakazi wa serikali walioadhibiwa au kufuatiliwa na vyombo vya sheria.

” Serikali ina nia ya kumaliza tatizo la kutoadhibu. Shirika letu la Folucon-F liliweza kuorodhesha zaidi ya askali polisi 150 hususan wajumbe wa SNR ( idara ya ujasusi) walioadhibiwa au kutolewa kwenye nyadhifa kutokana na tuhuma dhidi yao”, alisisitiza Gérard Hakizimana ambaye anakubali kuwa visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinaripotiwa nchini Burundi.

” Tunaomba mashirika hayo ya ndani ya nchi kutuonyesha mahala ambapo kuna watu hao ambao sisi tuliorodhesha kama watu waliouwawa. Shirika la Iteka haliridhishwi na kutoa ripoti zinazozungumzia watu waliouwawa. Tungependa kusema mambo mengine. Watuonyeshe mahala ambako kuna watu hao waliofariki au kutekwa nyara, tutafurahi kuwapata tena”, anajibu Anschaire Nikoyagize.

Shirika la Iteka linaomba serikali kuwahakikishia wananchi wote usalama na sheria kwa wote, na kuwajibika ipasavyo kwa kuwalinda wananchi na kufanya uchunguzi wa kiina ili kuwatafuta waliohusika na maovu na kuwapeleka mbele ya vyombo vya sheria bila kupendelea.

Kwa jamii ya kimataifa, shirika hilo linapendeleza juhudi za serikali ziungwe mkono. Jamii ya kimataifa inaombwa pia kuendelea kutumia ushawishi wake ili haki za binadamu ziweze kuheshimiwa kikamilifu nchini Burundi.

Previous Kuhusu-Bunyoni : kamanda wa kikosi cha kutuliza ghasia abadilishwa
Next Malawi: zaidi ya wakimbizi 400 kutoka nchi za maziwa makuu wakamatwa na polisi