Cibitoke : wafungwa wawili wafariki wakiwa katika gereza la polisi ya mkoa
Katika kipindi cha chini ya wiki moja, wafungwa wawili walifariki dunia wakiwa ndani ya gereza la kamishna ya polisi mkoani Cibitoke (kaskazini magharibi mwa Burundi). Msongamano ndani ya jela pamoja na ukosefu wa vyakula ndio chanzo cha vifo hivyo. Watetezi wa haki za binadamu wanaomba misaada kwa ajili ya wafungwa hao. Mwendeshamashtaka anahakikisha habari hizo lakini anasema ni mfungwa mmoja aliyefariki badala ya wawili. Anaomba msaada kwa ajili ya kuwasafirisha wafungwa ambao faili zao zilikamilika na ambao wanatakiwa kuhamishwa katika gereza kuu ya Bujumbura (mji wa kibiashara). HABARI SOS Médias Burundi
Wote wawili walikuwa na umri wa miaka takriban 30 na kuzuiliwa katika gereza la polisi katika mkoa huo tangu miezi mitatu iliyopita.
Mfungwa wa kwanza alifariki jumanne tarehe 5 septemba iliyopita, mwingine siku mbili badaye.
Kwa mjibu wa vyanzo mbali mbali, wahanga walikufa kutokana na ukosefu wa vyakula.
Mmoja kati ya wafungwa wenzake, alifahamisha kuwa kutokana na msongamano mkubwa wa wafungwa na ukosefu wa vyakula, idadi kubwa ya wafungwa hao wana dalili za maradhi ya utapia mlo na kula vibaya.
Mlinzi wa gereza alithibitisha habari hizo.
” Hakuna anayewaletea chakula. Wafungwa hao walikuwa katika ufukara bila kuwa na familia karibu inayoweza kuwaletea chakula sababu mmoja alikuwa kutoka tarafa ya Bukinanyana na mwingine mwenye asili ya tarafa ya Mabayi”, alibaini mlinzi huyo.
Mtetezi mmoja wa haki za binadamu alisisitiza juu ya swala la msongamano wa wafungwa.
” Mahabusu hao walituhumiwa makosa madogo madogo yanayohusiana na wizi katika makaazi ya watu. Idadi kubwa ndani ya gereza hilo lenye uwezo wa kuwapokea watu 20 na ambalo linawapa hifadhi wafungwa 130 husababisha mazingira mabaya ndani ya gereza ” alithibitisha.
Kwa mjibu wake, kama hakuna juhudi zozote, wafungwa wengine wanaweza kufariki dunia .
” Idadi kubwa ya mahabusu hao wanatuhumiwa makosa madogo madogo. Faili zao zisingechukuwa muda mrefu ndani ya kabati za majaji na OPJ. Ni budi kuongeza kasi katika kushughulikia kesi dhidi ya mahabusu wanaotuhumiwa madhambi madogo. Hali hiyo itasaidia katika kupunguza msongamano ndani ya gereza hilo ambalo halina viwango vya gereza ” alifahamisha.
Katika mahakama kuu ya mkoa wa Cibitoke, mwendeshamashtaka anahakikisha kifo cha mfungwa mmoja ambaye ” alifariki kutokana na maradhi ya muda mrefu”.
Hata hivyo, anakubali kuwa kuna msongamano mkubwa ndani ya gereza hilo. Kwa mujibu wake ukosefu wa gari kwa ajili ya kusafirisha wafungwa ambao adhabu zao zimejulikana ndio sababu. Anaomba washirika wao waliojikita katika sekta ya kutetea haki za binadamu kwa jumla na hususan kutetea haki za wafungwa kutoa msaada wa kuwasafirisha kuelekea gereza kuu ya Mpimba ndani ya mji mkuu wa kibiashara wa Bujumbura.