Kabarore: walimu walazimishwa kutoa michango

Kabarore: walimu walazimishwa kutoa michango

Walimu katika tarafa ya Kabarore mkoa wa Kayanza (Kaskazini mwa Burundi) walilazimishwa kutoa michango ya pesa ili kufadhili miradi ya chama tawala cha CNDD-FDD. Wahusika wanatupilia mbali kile wanachoita “ukiukwaji wa haki za binadamu”. HABARI ya SOS Medias Burundi

Tangu mwaka wa 2015, walimu katika baadhi ya tarafa za Kayanza wanalazimishwa kutoa michango kwa nguvu ili kufadhili miradi ya chama tawala nchini Burundi. Tarafani Kabarore, walezi hawachangii tena.

Vyanzo vyetu katika walimu wanatuarifu kuwa michango hiyo ni ya kila mwezi.

Walimu wakuu wa shule za msingi wanatoa kati ya 5000 na 10000 sarafu ya Burundi kutokana na idadi ya wanafunzi kwenye shule hiyo.

“Sisi walimu tunatoa elfu moja au elfu mbili. Kwa kipindi fulani walitulazimisha kutoa elfu 3 sarafu za Burundi, alieleza mwalimu.

Jambo la kusikitisha kwa mjibu wa walimu, hakuna anayeepukika.

“Hata wafuasi wa vyama vingine wanahusishwa”, anahakikisha mwalimu mwengine.

Wanaopinga kuchukuliwa kama wasiokuwa na utu.

“Mara tunaitwa mbwa , mara tunapewa jina la mbwa mwitu”, alithibitisha mwalimu mufuasi wa chama cha upinzani.

Walimu wanasema kuchoshwa na michango hiyo hasa ikizingatiwa kuwa hawajuwi inapoelekea pesa hiyo.

“Hakuna matokeo kutoka kwenye michango yetu”, analaani mwalimu mkuu wa shule, mufuasi wa chama tawala cha CNDD-FDD.

Walimu waliojieleza kwenye SOS Medias Burundi wanataja kuwa kuchangisha kwa nguvu ni “ukiukwaji wa haki za binadamu”. Wanaomba serikali na viongozi wa chama cha CNDD-FDD kwa ngazi ya taifa kuingilia kati na kusimamisha mwenendo huo.

Viongozi wa elimu katika mkoa wa Kayanza, hawakupatikana ili kujieleza juu ya madai hayo.

Previous Makamba: Vijana Imbonerakure wahamishwa nje ya shule ya Makamba
Next Muyinga: Zaidi ya wapinzani 50 wanazuiliwa jela