DRC: Maï Maï wanataka kusaidia jeshi la FARDC

DRC: Maï Maï wanataka kusaidia jeshi la FARDC

Makundi mbali mbali ya Maï Maï yalifahamisha kuwa yanataka kushirikiana na jeshi la Kongo katika vita dhidi ya kundi la M23. Hii ni baada ya rais Tshisekedi siku ya alhamisi kuwatolea wito raia wake kuungana dhidi ya “uvamizi wa Rwanda”. Ujumbe huo ulisambazwa na wawakilishi wa mashirika ya kiraia ya nchi hiyo kubwa ya afrika ya kati. HABARI SOS Médias Burundi

Matawi mbali mbali ya Maï Maï yanayofanyia operesheni zake katika mkoa wa kivu-kusini, kivu-kaskazini na Maniema mashariki mwa DRC yanaomba jeshi la FARDC kuwaacha wasaidie katika mapambano dhidi ya kundi la M23″. Matawi yaliyokwisha onyesha nia hiyo ni Maï Maï René, Bilozebishambuke, Malaika, Makanaki, Buhirwa, Nyatura na Raia mutomboki.

” M23 inatakiwa kupigwa vita na raia wote wa Kongo kama mtu mmoja. Ni haki yetu kufanya hivyo na tuko katika mazungumzo na makundi mengine ya silaha ili kufanikisha jukumu hilo”, alifahamisha René Itongwa muwakilishi wa Maï Maï René.

Msemaji wa jeshi la Kongo Kivu-kusini Luteni Marc Elongo anasema kuwa ” FARDC haina nia ya kushirikiana na makundi ya Maï Maï sababu jukumu lake ni kutokomeza makundi yote ya waasi”.

Kivu-kaskazini ambapo kundi la M23 linaendelea kusonga mbele, makundi ya Maï Maï Mutomboki na Maï Maï Nyatura yalitangaza kuwa ” tunashirikiana na FARDC katika vita dhidi ya M23″.

Wakati huo huo, angalau vijana elfu 3 tayari walijiorodhesha kujiunga na jeshi tangu wito wa rais kwa vijana hao ” kujiunga na jeshi la FARDC ili kulinda taifa letu dhidi ya uvamizi wa Rwanda katika vita hiyo tulioyazimishwa na majirani”.

Baadhi waliwambia wandishi wa habari kuwa wanataka kuiga mfano wa vijana wa Ukraine ambao waliacha kila kitu na kulihami taifa lao.

Wadadisi waliwataja makurutu hao ni kama “Nyama laini” FARDC ikiwa ilishindwa kuwarudisha nyuma waasi wa M23 waliochukuwa udhibiti wa maeneo mengi ndani ya Kivu-kaskazini katika siku chache zilizopita.

M23 ni kundi la zamani la waasi wa kabila la watutsi lililochokuwa silaha 2021, linatuhumu viongozi wa Kongo kwa kutoheshimu ahadi zake za kuwarejesha katika maisha ya kawaida wapiganaji wake.

Serikali ya Kongo imekuwa ikituhumu Rwanda kuunga mkono kundi hilo la waasi, jambo ambalo viongozi wa nchi ya Rwanda walikanusha daima badala yake jeshi la Kongo likituhumiwa kushirikiana na kundi la waliofanya mauwaji ya halaiki la FDLR kwa lengo la kuvuruga utawala wa Rwanda.

Previous Kigali (Rwanda): renewal of identity cards for refugees and reception of new asylum applications
Next Cibitoke: general increase in basic necessities