Goma: ma mia ya visa vya ubakaji yaripotiwa eneo la Kanyarutchinya
Visa vya unyanyasaji wa kijinsia viliongezeka katika kijiji cha Kanyarutchinya wilayani Nyiragongo na Bulengo magharibi ya mji wa Goma Kivu kaskazini tangu kuibuka tena kwa kundi la M23. Viongozi wa kambi ya wakimbizi wa ndani wanasema visa 402 viliorodheshwa tayari. Idadi kubwa ya waathiriwa ni wakimbizi wa ndani walitoroka mapigano kati ya M23 na jeshi la FARDC (jeshi la jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo). HABARI SOS Médias Burundi
Akinamama wakimbizi wa ndani kila siku wanaelekea eneo la Munigi kwa ajili ya kuchukuwa unga wa kutengeneza uji. Kawaida kunakuwa na mlolongo mrefu wakisubiri kupewa. Ni budi kuamka mapema ili kuweza kupata uga huo. Ni kwenye njia hiyo ambapo wanakuta watu wenye silaha ambao wanawanyanyasa.
Mkuu wa kambi ya Kanyarutchinya Théo Museruka anasema kuwa tayari waliorodhesha visa 402 vya akinamama walionyanyaswa kijinsia.
” Baadhi walinyanyaswa wakati wa wakitembea. Lakini sehemu kubwa ya uvamizi huo ulifanyika wakati wa shughuli za akinamama hao nje ya kambi. Mara nyingi wanabakwa usiku au nyakati za asubuhi mapema wakati wakielekea kutafuta chakula ndani ya kambi ” alibaini.
Kulingana na takwimu za shirika la MSF( waganga wasiokuwa na mipaka), kati ya mwezi julai na disemba mwaka jana wanawake 262 walipokelewa kwenye kituo cha afya cha Kanyarutchinya.
” Tangu mwaka wa 2023 katika kipindi cha wiki sita peke , akinamama 155 eneo la Kanyarutchinya pamoja na 188 eneo la Munigi waliripoti kwa timu za wauguzi baada ya kunyanyaswa kijinsia ” , shirika hilo lilizidi kufahamisha.
Itafahamika pia kuwa tarehe 24 februari iliyopita, shirika la MSF liliwapokea akinamama 143 kwenye kituo cha Tumaini wakiwemo 47 katika kipindi cha siku tatu peke.
Mwanzoni mwa mwezi februari uliopita, wanawake wengi waliandamana katika barabara za mji wa Goma kwa ajili ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia. Waliomba serikali ya Kongo kurejesha amani katika mkoa wa kivu kaskazini.
Hivi karibuni, mashirika ya akinamama pamoja na viongozi wa mashirika ya kiraia katika mkoa wa Kivu kaskazini, walituhumu kundi la M23 kuhusika na visa vya ubakaji dhidi ya ma mia ya akinamama katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Lakini msemaji wa kundi hilo la waasi meja Willy Ngoma alipinga madai hayo.
” Ni lazima mujiulize swala hili: Nani alifanya uchunguzi ? akinamama hao walibakwa eneo gani? Siku gani ? Mutagundua kuwa sio madili yetu. Kwa nini hatukubaka eneo la Bunagana ? kwa nini hatukufanya hivyo eneo la Kiwanja? Kwa nini hatukubaka katika miji mikuu ambayo ninataja hapa kama Rutshuru….na kwenda kubaka eneo la Kishishe…. sijuwi wapi…”, alijitetea.
Na kuendelea na maelezo ” Sisi jeshi la mapinduzi la Kongo, tulimaliza miaka minne nchini Uganda ndani ya kambi ya kijeshi. Ulizeni maswala raia wa Uganda. Tulikuwa katika eneo ambako kuna wanawake wazuri, Banyankole. Kwa kipindi cha miaka minne, jeshi la mapinduzi la Kongo halikuwahi kubaka hata msichana mmoja. Ulizeni swala hilo raia wa Uganda. Ni maeneo wanayosema ili kutuchafua na baadhi ya mashirika malengo yao ni kutafuta noti za benki. Ni uongo mtupu. M23 haiwezi kamwe kubaka mwanamke”.
Novemba iliyopita, viongozi wa Kongo walituhumu M23 mauwaji ya angalau wananchi wa kawaida 272 katika eneo la Kishishe ndani ya mkoa wa Kivu kaskazini. Wizara ya Kongo ya sheria ilipeleka mashtaka katika mahakama ya uhalifu wa kimataifa ICP siku chache badaye ikituhumu waasi haonkadhalika na Rwanda.
Kundi la M23 liliomba uchunguzi huru ufanyike kuhusiana na mauwaji hayo na kutuhumu viongozi wa Kongo ” nia ya kuondoa uaminifu wa kundi hilo mbele ya wananchi”.