Goma : miili ya watu zaidi ya arobaini yazikwa kwa amri ya serikali licha ya upinzani wa familia na mashirika ya kirai

Goma : miili ya watu zaidi ya arobaini yazikwa kwa amri ya serikali licha ya upinzani wa familia na mashirika ya kirai

Angalau miili ya watu 40 ilizikwa jumatatu hii tarehe 18 septemba 2023 kwa amri ya gavana wa mkoa wa kivu kaskazini mashariki mwa jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo licha ya upinzani mkubwa wa wajumbe wa familia ambao wanaomba uchunguzi ufanyike kabla ya mazishi. Tarehe 30 agosti iliyopita, zaidi ya watu 50 waliuwawa na wanajeshi wa Kongo wakati wa mandamano dhidi ya Monusco (ujumbe wa umoja wa mataifa nchini DRC). HABARI SOS Medias Burundi

Makundi ya wananchi pamoja na vikundi vingine vya shinikizo walitangaza kufanya mandamano ili kutoa heshma kwa wananchi waliouwawa tarehe 30 agosti. Kwa mjibu wa wakaazi mjini Goma, meya alipinga mandamano hayo.

Gavana wa mkoa wa kivu kaskazini jumatatu hii alitoa amri ili watu hao wafanyiwe mazishi licha ya upinzani wa familia za wahanga ambao wanatoa baadhi ya masharti kabla ya mazishi. Wanatuhumu viongozi wa mkoa kukataa ushirikiano na familia.

Kwa mjibu wa vyanzo vya kijeshi, mahakama ya kijeshi mjini Goma inafanya kila liwezekanalo ili kuwatambua waliofanya mauwaji hayo ya wananchi katika mji mkuu wa mkoa wa kivu kaskazini.

” mimi sikubaliani na viongozi wetu ambao wamewazika watu wetu bila kutushirikisha. Inamaanisha kuwa nia yao ni kutaka kupoteza ishara zote zinazoonyesha namna ma kaka na ma dada zetu, na wazazi wetu walivyouwawa. Tunaomba wale ambao wanazuiliwa jela hapa mjini Goma waweze kuachiliwa huru na badaye yafanyike mazishi ya heshma” ndugu wa muhanga mmoja aliambia SOS Medias Burundi .

Mashirika ya kiraia upande wake yanafikiria kuwa viongozi wa kijeshi kwa ushirikiano na serikali kuu ya Kinshasa walitumia utawala wao ili kukiuka haki za raia wa Kongo.

” hakika hatuna uaminifu kwa serikali yetu. Vipi unaweza kumuzika mtu bila kushirikisha familia yake? Ni ukiukwaji wa haki za raia wa kongo na tunaomba vyombo vya sheria vya kongo kama sio washirika kuanzisha uchunguzi wa kina ili gavana mwanajeshi Constant Ndima Kongba na wajumbe wa serikali yake waweze kuwajibishwa kuhusu maovu waliotenda “, anadai Ciceron Denis kiongozi wa mashirika ya kiraia nchini Kongo katika mji wa Goma.

Ikumbukwe kuwa mauwaji ya tarehe 30 agosti iliyopita yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 50 idadi kubwa ikiwa ni vijana wajumbe wa dhehebu la dini ya kienyeji eneo hilo.

Previous Burundi : ni lazima iwepo sera ya misharaha inayovutia ili kuwazuia waganga kwenda nje ya nchi (Chama cha wafanyakazi)
Next Rwanda: Paul Kagame atangaza kugombea urais mwaka wa 2024