Burundi : ni lazima iwepo sera ya misharaha inayovutia ili kuwazuia waganga kwenda nje ya nchi (Chama cha wafanyakazi)

Burundi : ni lazima iwepo sera ya misharaha inayovutia ili kuwazuia waganga kwenda nje ya nchi (Chama cha wafanyakazi)

Mishahara midogo pamoja na ukosefu vifaa vya kutosha ndio sababu kuu ya waganga wa Burundi kutoroka na kwenda kuhudumu katika nchi zingine. Ni tamko la kiongozi wa chama cha kutetea haki za wafanyakazi wa sekta ya afya (SYNAPS). Alitoa kauli hiyo katika mkutano na wandishi wa habari alhamisi iliyopita. Anaomba serikali kufanya juhudi na kutekeleza sera nzuri ya mishahara na kumaliza tatizo hilo linalozidi kuwa na kasi. Wizara ya afya ilijieleza mbele ya bunge la taifa. HABARI SOS Medias Burundi

Daktari Vincent Ndayizigiye alifahamisha kuwa hali hiyo ya waganga kutoroka nchi inaweza kusababisha madhara makubwa mathalan vifo kuongezeka ndani ya hospitali na sekta ya afya kurudi nyuma.

Akiwa kati kati ya wajumbe wa chama cha kutetea haki za ma daktari nchini Burundi ( SYMEGEB), kiongozi wa chama cha wafanyakazi SYNAPS alisema kuwa mshahara wa kila mwezi haufiki laki tano sarafu za Burundi kwa idadi kubwa ya waganga.

” hali hiyo bila shaka inawapelekea kwenda kutafuta maisha mazuri kwingine ambapo watalipwa vizuri “, alisisitiza.

Kwa mjibu wa daktari Ndayizigamiye, kuna uwezekano kwa vijana wa Burundi kupoteza moyo wa kusoma masomo marefu ya uganga.

” Hatari nyingine ni kwamba waganga ambao wanasalia nchini, watafanya kazi katika sekta binafsi ambapo mbali ya kupata mishahara mizuri, watapata pia vifaa vizuri ili kuweka vitendoni yale waliosomea “, alizidi kusema mganga huyo.

Kulingana na vyama hivyo viwili, serikali ingelivalia njuga swala hilo ili kuokoa maisha ya wananchi ambayo yanaweza kuathiriwa katika siku zijazo kwa kulipa gharama kubwa ndani ya hospitali za kibinafsi wakitafuta huduma nzuri.

Wanazidi kusema kuwa ni budi serikali kulipia masaa ya ziada ili kuwapa moyo waganga kusalia kazini.

Takwimu

Waziri wa afya Sylvie Nzeyimana alialikwa bungeni ili kujieleza kuhusu utoro mwingi wa waganga wa sekta ya umma.

” waganga 130 kutoka vituo vya afya 80 walikwenda kufanya kazi nje ya Burundi ” alisisitiza waziri akitaja ripoti ya mwaka wa 2021iliyotungwa na wizara yake. Ilikuwa jumanne hii katika mji mkuu wa kibiashara Bujumbura.

Kulingana na vyanzo vya kiganga vilivyozungumza na SOS Medias Burundi nchini Rwanda na Kenya, angalau waganga 150 wa Burundi walipokelewa nchini Rwanda tangu 2014, Kenya ikiwa iliwapokea zaidi ya 50 tangu wakati huo.

Waganga wengine wenye asili ya Burundi wanaelekea nchini Ufaransa mnamo siku hizi, vyanzo katika sekta ya kiganga vilihakikishia SOS Medias Burundi.

Previous Cibitoke: wanajeshi sita wasimamishwa baada ya kupurukushana na Imbonerakure
Next Goma : miili ya watu zaidi ya arobaini yazikwa kwa amri ya serikali licha ya upinzani wa familia na mashirika ya kirai