Fizi : mapigano kati ya kundi la Mai Mai na Twirwaneho
Mapigano makali yanaripotiwa tangu asubuhi ya jumatatu hii kati ya kundi la Mai Mai Biloze Bishambuke dhidi ya wapiganaji wa kundi la silaha la Twirwaneho linaloundwa na vijana Banyamulenge. Makundi hayo yanatuhumiana uchokozi. Mapigano yamefanyika katika wilaya ya Fizi mkoa wa Kivu-kusini mashariki mwa DRC. Wakaazi wengi wanaoundwa na jamii za Bafulero na Babembe wanaoishi katika eneo hilo wamelazimika kutoroka makaazi yao kutokana na mapambano hayo. HABARI SOS Médias Burundi
Ni katika eneo la Lulenge ambapo mapigano makali yameripotiwa.
” Leo katika maeneo tofauti ya sekta ya Lulenge katika wilaya ya Fizi mkoa wa Kivu kusini , mapigano makali yameibuka kati ya kundi la Twirwaneho na Mai Mai , ameambia SOS Médias Burundi Aimable Nabulizi, msemaji wa kundi la Mai Mai Biloze Bishambuke. Anahakikisha kuwa waasi wa Twigwaneho na Gumino walishambulia vijiji vya Musika, Kijombo, Lubinjila na Busheke na kuchoma moto nyumba na kuuuwa watu na kupora ng’ombe”.
Vyanzo vya ndani vinathibitisha kuwa mapigano kati ya kundi la Mai Mai na Twirwaneho yamefanyika.
” Ng’ombe wengi wameibiwa “, wakaazi wametuhumu wapiganaji wa jamii ya Banyamulenge kushambulia ngome za kundi la Mai Mai.
Kupitia tangazo, kundi la Twirwaneho linatuhumu lile la Mai Mai Biloze Bishambuke na Red Tabara , kundi la silaha la warundi, kutoka eneo la Musika na kuelekea kushambulia vijiji vya Banyamulenge wa Rutigita, Masha na Monyi”.
Kundi la Twirwaneho linafahamisha kuwa limerudisha nyuma shambulio hilo. Baadhi ya mashirika huru yanayofanyia kazi katika sekta ya Lulenge wanasema kuwa ni kundi la Twirwaneho lililoshambulia vijiji vya Musika na Kijombo.
” Wananchi wengi wametoroka makaazi yao na kuelekea maeneo la Karambi na Mimbiriro ( katika sekta hiyo) kwa ajili ya kutafuta hifadhi”, wananchi hao wameambia wandishi wa SOS Médias Burundi.
Msemaji wa kundi la Mai Mai Biloze Bishambuke anadai kuna waasi wa M23 waliowasili katika mkoa wa Kivu ya kusini tangu mwishoni mwa wiki iliopita.
” Wako katika milima mirefu na mabonde ya wilaya ya Fizi, Uvira, Mwenga/Itongwe na walipokelewa na makundi ya silaha ya Banyamulenge wanaoungwa na Rwanda, anatuhumu bwana Nabulizi.
Hata hivyo, wandishi wetu katika mkoa wa Kivu ya kusini na kaskazini, wamegundua kuwa kundi la M23 halijafunga safari ya kuelekea Kivu ya kusini licha ya kuonekana karibu na mpaka wa mikoa hiyo miwili ya mashariki mwa Kongo huku mapigano ya wiki iliyopita yakilenga kudhibiti Minova, eneo la mpakani upande wa Kivu kusini.
Mapigano hayo yalifanyika wakati ambapo jumapili hii tarehe 12 machi, jeshi la Burundi kwa ushirikiano na kundi la Mai Mai Masango walishambulia na kupora ng’ombe eneo la Muramvya (daima katika mkoa wa Kivu kusini) na kumuuwa mkaazi mmoja kulingana na vyanzo vya ndani. Hakuna tamko rasmi la FDNB ( jeshi la Burundi ), FARDC ( jeshi la jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo ) pamoja na kundi hilo kuhusu madai hayo.