Cibitoke : Zaidi ya wafungwa 180 ndani ya gereza ndogo ya polisi

Cibitoke : Zaidi ya wafungwa 180 ndani ya gereza ndogo ya polisi

Watu 178 wanazuiliwa ndani ya gereza ya kamishna ya polisi mkoani Cibitoke (kaskazini magharibi mwa Burundi) ambayo ina urefu wa mita 8 kwa upana wa mita 4. Idadi kubwa ya mahabusu hao wanafuatiliwa kwa makosa madogo madogo kama wizi ndani ya mashamba na makaazi. Watetezi wa haki za binadamu wanalaani mazingira hayo ya kifungo. HABARI SOS Médias Burundi

Gereza hiyo ambayo ilijengwa na CICR (shirika la kimataifa la msalaba mwekundu) , ina uwezo wa kuwapokea wafungwa 25 peke. Kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali, watu wanaozuiliwa katika gereza hilo wako katika mazingira mabaya.

” Wanakosa vyoo na choo kimoja kinatumuwa na umati huo wote”, chanzo cha polisi kinafahamisha.

Wafungwa wanapeana zamu ili waweze kulala. Baadhi wanalala wakiwa wamesimama na chini kwenye ardhi. Athari ni nyingi ikiwa ni pamoja na maradhi ya utapia mlo kwa idadi kubwa ya wafungwa ambao wanasumbuka kupata chakula kutokana na msongamano wao.

Kama alivyoweza kushuhudia mwandishi wetu eneo hilo, msongamano wa wafungwa unatokana na sababu nyingi.

Gereza hiyo ni moja inayomilikiwa na mkoa huo na kuwapokea wafungwa wote kutoka tarafa sita za mkoa huo wa Cibitoke.

Chanzo katika polisi ki naitaja hali hiyo kuwa ni ngumu. Chanzo hicho kinafahamisha kuwa idadi kubwa ya watu wanaoepuka hali ya wananchi kujichukulia sheria wanaletwa ndani ya gereza hilo bila kuheshimu utaratibu kisheria.

Sababu nyingine ya msongamano huo kulingana na jaji alikuwa eneo hilo, ni kuchelewa kwa utaratibu wa kisheria na kufanya muda mwingi.

Mwanasheria huyo anatoa mfano wa baadhi ya wafungwa waliohukumiwa ambao wamemaliza kati ya miezi mitatu na sita wakati ambapo wangetakiwa kupelekwa katika gereza kuu ya Mpimba ( mji wa kibiashara) .

Hali hiyo inawakasirikisha watetezi wa haki za binadamu. Mmoja wao alisema wazi kuwa ” mazingira ya gerezani yanatakiwa kuheshimu viwango vya heshma kwa binadamu”.

Anaomba wizara ya sheria kutafuta suluhu ya tatizo hilo ambalo limedumu na hivyo kukiuka haki za wafungwa.

Mwendeshamashtaka katika korti kuu ya mkoa wa Cibitoke anafahamisha kuwa ” ukosefu wa gari kwa ajili ya kuwapeleka wafungwa mjini Bujumbura ndio sababu ya msongamano ndani ya gereza”.

Anaomba mashirika ya kihisani ambayo yanahudumu katika sekta ya haki za binadamu na wadau wengine ” kuwasaidia kwa kuhakikisha usafiri wa wafungwa hao”.

Kulingana na kauli yake, ni kawaida kuchukuwa hatua za kuwaachilia huru wafungwa ili kupunguza msimamo lakini hali hiyo haibadiliki.

Akihojiwa kuhusiana na hali hiyo, gavana wa mkoa wa Cibitoke, alifahamisha kuwa anataraji kuongoza mkutano kati ya viongozi wa sekta ya sheria na polisi ili kujaribu kuchukuwa hatua kukabiliana na changamoto hiyo.

Previous DRC (Kivu kaskazini) : shughuli zaanza pole pole kwenye mpaka wa Bunagana
Next Uvira : watu wawili wauwawa