Kivu-kaskazini : akinamama zaidi ya mia moja walibakwa na waasi wa M23 (mashirika ya kiraia)

Kivu-kaskazini : akinamama zaidi ya mia moja walibakwa na waasi wa M23 (mashirika ya kiraia)

Shirika la akinamama wakimbizi wa ndani lilifahamisha kuwa zaidi ya akinamama mia moja walibakwa na waasi wa M23. Wiyala za Rutshuru, Nyiragongo na Masisi ndani ya Kivu kaskazini (mashariki mwa DRC) zinakabiliwa zaidi na vurugu hizo kutokana na mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23. Msemaji wa kundi la M23 anapinga madai hayo ambayo hata hivyo yanafichuliwa na mashirika ya kiraia ya eneo hilo. HABARI SOS Médias Burundi

Akinamama wengi eneo hilo wanadai kuathiriwa na ubakaji unaofanywa na waasi wa M23.

“Tunateseka. Waasi wa M23 wanatunyanyasa kijinsia. Wakati tukienda shambani, waasi wanatubaka . Kwa hiyo hatuwezi tena kuendesha kilimo kwenye ardhi zetu. Warudi kwao ” alitoa ushuhuda huo M.R, mwanamke kutoka wilaya ya Rutshuru.

Kwenye kitongoji cha Bukombo, katika kijiji cha Bwito ndani ya wilaya ya Rutshuru, akinamama wakiwemo wale wa zaidi ya miaka 60 walibakwa, kisha wakauwawa na waasi wa M23 eneo la Gashavu chini ya udhibiti wao , vyanzo eneo hilo vinaripoti.

Héritier Gashegu, mtetezi wa haki za binadamu katika ukanda huo, anasema kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kiutu.

” Wanawake wawili walibakwa eneo la Gashavu na mmoja alikatwa kichwa na kuchomwa eneo la Kazuba ndani ya kitongoji cha Bukombo”, anadai mwanaharakati huyo.

Akimama wakimbizi wa ndani ndio wa kwanza kuathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia , kulingana na mashirika ya akinamama eneo hilo.

Hali hiyo inalaaniwa vikali na akinamama wakimbizi wa vita eneo la Kivu kaskazini.

” Tunalaani vikali ubakaji dhidi ya akinamama na wasichana. Zaidi ya akinamama mia moja walibakwa na waasi wa M23 wakiwemo akinamama wawili wakongwe ( miaka kati 60 na 70), na badaye wakauwawa na waasi wa M23″, alihakikisha Claudine Neema, muakilishi wa akinamama wakimbizi wa ndani katika eneo hilo la Kongo.

Unyanyasaji dhidi ya akinamama ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kiutu, aliendelea kusema.

Shirika linalodai kuwa la ushahuri na kulinda haki za binadamu na watoto linasema kuwa liliorodhesha raia wa kawaida 482 waliouwawa wakiwemo akinamama 185 tangu ujio wa kundi la M23 eneo la Kivu kaskazini.

Meja Willy Ngoma msemaji wa jeshi la M23 katika mahojiano na SOS Médias Burundi atakanusha madai hayo.

[….] Jiulizeni maswala yafuatayo: Nani alifanya uchunguzi huo? Akinamama hao walibakwa wakiwa wapi? Siku gani ? Mtaona kuwa sio mwenendo wetu. Vipi hatukubaka eneo la Bunagana ? Kwa nini hatukubaka eneo la Kiwanja ? kwa nini hatukubaka kwenye makao makuu ya Rutshuru….Je tutakwenda kubaka eneo la Kishishe…. sijuwi wapi “, alizidi kuuliza.

Na kuendelea kutoa maelezo” sisi jeshi la mapinduzi ya Kongo, tulifanya miaka minne nchini Uganda ndani ya kambi ya kijeshi. Ulizeni swali watu wa Uganda. Tulikuwa katika eneo ambako kuna wasichana wazuri, Kabila la Banyankole. Kwa miaka minne, jeshi la mapinduzi la Kongo halikubaka hata msichana mmoja . Ulizeni raia wa Uganda. Ni mambo wanayosema ili kutuchafua na baadhi ya mashirika ya kiraia yanatafuta pesa. Ni uongo mtupu. M23 haiwezi kuwabaka akinamama hao”.

Mwishoni mwa novemba 2022, viongozi wa Kongo walituhumu kundi la M23 kuwauwa angalau raia wa kawaida 272 katika eneo la Kishishe eneo la kivu kaskazini. Waziri wa sheria wa Kongo alipeleka mashtaka katika korti ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) siku chache badaye waasi hao pamoja na Rwanda walituhumiwa kutekeleza mauwaji hayo.

Kundi la M23 lilikuwa limeomba uchunguzi huru ufanyike kuhusu mauwaji hayo na kutuhumu viongozi wa Kongo ” nia ya kuwachafua mbele ya wananchi”.

Previous Bujumbura : watetezi watano wa haki za binadamu waripoti mahakamani
Next Burundi : Ndabirabe na tathmini yake ya sera za kiuchumi na kisiasa