Goma : angalau watoto 16 walifariki dunia kutokana na mazingira mabaya ndani ya kambi mpya ya wakimbizi wa ndani ya Majengo

Goma : angalau watoto 16 walifariki dunia kutokana na mazingira mabaya ndani ya kambi mpya ya wakimbizi wa ndani ya Majengo

Watoto wote 16 walifariki dunia katika kipindi cha chini ya wiki mbili. Kituo kinachowapa hifadhi wakimbizi hao wa vita kinapatikana katika kata ya Majengo tarafa ya Karisimbi. Ni katika mji wa Goma makao makuu ya mkoa wa Kivu kaskazini mashariki mwa jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Habari hizo zimethibitishwa na mashirika ya kiraia, makanisa pamoja pia na mkuu wa kambi hiyo ya wakimbizi wa ndani. Wanalaani mazingira hayo mabaya na kuilaumu serikali kwa kuacha kuwasaidia wakimbizi wa ndani tangu walipotoroka maeneo yao ya asili na kutafuta hifadhi eneo hilo. HABARI SOS Médias Burundi

Kambi hiyo mpya ya wakimbizi wa ndani kata ya Majengo inawapa hifadhi zaidi ya Kaya 280. Mazingira ya maisha ni mabaya kama ilivyo kwa wakimbizi wengine walioomba hifadhi katika mji wa Goma. Mazingira ya maisha yao ni magumu.

” Tunaomboleza vifo vya zaidi ya watoto 15 katika kipindi cha chini ya wiki mbili. Lakini tunashuhudia kuwa viongozi wetu hawajali kamwe maisha ya kila siku ya raia wa Kongo wanaoishi katika mazingira mabaya kiafya. Watoto hao walifariki kutokana na mazingira mabaya ya maisha “, alitahadharisha Munago mmoja kati ya viongozi wa sehemu ya kambi hiyo.

Vifo vya watoto hao wakimbizi wa ndani vinawasikitisha pia watetezi wa haki za binadamu katika mkoa wa Kivu kaskazini.

” ni jambo lisiloeleweka watoto wakifariki bila msaada wowote wa viongozi wa Kongo. Hiyo inamaanisha kuwa haki za watu wenye matatizo hazizingatiwi na viongozi wa Kongo. Tunaomba viongozi wa Kongo kuthibitisha kuwa wanajali maisha ya raia wa Kongo ” , alikumbusha John Bahati mwanaharakati wa shirika la kiraia la Force vive mkoa wa Kivu kaskazini.

Waliopewa hifadhi ndani ya kambi hiyo ni watoto lakini pia na watu wenye umri mkubwa. Ni wenye asili ya maeneo mbali mbali ya wilaya ya Nyiragongo na sehemu ya Rutshuru kutokana na mapigano kati ya jeshi la Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23.

Wakimbizi hao wahakikisha kuwa hawajapata msaada wowote kutoka kwa viongozi wa Kongo au kutoka kwa mashirika yanayojihusika na watu wanaokabiliwa na matatizo wanaohudumu katika eneo hilo la mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

” Tunapita katika nyakati ngumu ndani ya kambi ya wakimbizi wa ndani hapa kwenye kanisa la CBCA ( jumuiya ya Baptiste eneo la kati kati mwa Afrika)-MAJENGO. Nilifika hapa wiki mbili zilizopita, na bado hatujapata chochote kutoka kwa viongozi wetu” , alilalamika Ange Malimingi mwanamke aliyezungumza na SOS Médias Burundi.

Baadhi ya wakimbizi wanakiri kuwa walipata msaada wa vyakula kutoka kanisa la CBCA. Wakimbizi walipewa hifadhi ndani ya Majengo ya kanisa hilo.

Mara ya mwisho tulipata msaada kutoka kwa viongozi wa kanisa la CBCA Majengo. Tunawashukuru sababu msaada wao ulitufariji, alifahamisha Mugarura Habimana mmoja kati ya wakimbizi kutoka Kibumba.

Kwa mjibu wa viongozi wa kanisa, msaada huo bado hautoshi kukidhi mahitaji ya wakimbizi waliopewa hifadhi ndani ya majengo ya kanisa.

Mchungaji Senzoga Patrick anatoa wito kwa serikali ili iweze kuingilia kati haraka.

” Ni kweli tuliwapa msaada mdogo sababu tuliwapokea. Lilikuwa jambo lisilokubalika kuona watu wakifariki kutoka na na njaa mbele yetu sababu ni sisi tunaoishi kila siku na wao. Lakini hadi sasa msaada tunaowapatia ni mdogo. Tunaomba viongozi wa Kongo kufanya kila liwezekanalo ili kuwasaidia raia hawa wa Kongo wanaokabiliwa na nyakati ngumu”, alizidi kusema.

Kati ya wakimbizi hao, baadhi walitoka katika kambi ya Kanyarutchinya na Don Bosco wakihofia mazingira magumu kutokana na hali mbaya ya kiafya.

” Mimi nilikuja hapa lakini kabla, nilikuwa katika kambi ya Kanyarutchinya. Niliondoka kutokana na mazingira mabaya ya kiafya. Watoto wangu wote wanne walikufa kutokana na maradhi ya uchafu. Nilijiuliza kuwa zamu yangu inakaribia kufika. Nilipatwa na msongo wa mawazo baada ya kupoteza watoto wangu. Kabla ya kufika hapa mume wangu aliuwawa katika mapigano kwetu eneo la Jomba mwezi juni” , alibaini Emelyne Batachoka.

Wasi wasi unatoka katika pande zote

Kwa sasa mji wa Goma unazungukwa na kambi za wakimbizi upande wa kaskazini na kusini. Na hali hiyo ni hatari kubwa kwa wakaazi wa mji huo. Wakaazi hao wanahofia kupatwa na maradhi yanayosababishwa na usanifishaji mdogo kutokana na kambi hizo ambapo usafi haukuzingatiwa.

Wakimbizi wanaishi katika mazingira ambayo na wenyewe wanasema ni mabaya.

Mfano ni kambi ya Bulengo ambayo mbali ya kukabiliwa na athari za gesi aina ya méthane kutoka ziwa la Kivu, wakimbizi wanakabiliwa pia na ukosefu wa misaada ya kiutu. Wakimbizi idadi kubwa ni kutoka wilaya ya Masisi. Walitoroka mapigano makali kati ya jeshi la FARDC na kundi la M23 katika kitongoji cha Bashali na Bahunde ambapo maeneo mengi yanadhibitiwa na waasi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu mashariki mwa DRC yalilaani ukosefu wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wakimbizi wa ndani ya kambi za Goma na Nyiragongo.

Mji wa Goma unaorodhesha kambi tatu za wakimbizi wa ndani ikiwemo kambi ya Bulengo katika kata ya Lac vert kusini magharibi ya mji katika tarafa ya Goma , kambi ya Don Bosco katika kata ya Kasika tarafani Karisimbi pamoja na kambi ya Majengo katika kata ya Majengo daima katika tarafa ya Karisimbi

Previous Mabanda : mwanaume mmoja aishi kwa kujificha akihofia kuuwawa na viongozi wa chama cha CNDD-FDD
Next Rwanda-Burundi : michezo kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za polisi