Cibitoke: miili mingine imepatikana tarafani Rugombo

Cibitoke: miili mingine imepatikana tarafani Rugombo

Jumatatu hii miili mingine imegunduliwa na wakulima wa pamba kwenye transversale 8 ya kitongoji na Kijiji cha Cibitoke tarafani Rugombo mkoa wa Cibitoke ( kaskazini-magharibi mwa Burundi). Wakaazi wanasema kusitikishwa na upatikanaji huo wa maiti. Kwa jumla miili 19 ilipatikana katika tarafa jirani za Rugombo na Buganda . Wakaazi wanaomba uchunguzi ufanyike. Viongozi tawala wanasema kuwa utambulisho wa wahanga hao bado kujulikana. HABARI SOS Médias Burundi

Mashahidi wanasema kuwa wakulima wa pamba walikuwa wakielekea shambani kufanya kazi yao ya kila siku na kuona miili miwili ya wanaume wawili waliofungwa kamba. Walikuwa wakizungukwa na nzi wengi, ilikuwa kwenye transversale 8 kitongoji cha Cibitoke.

” Tulitoa taarifa kwa wanajeshi wa kituo cha Karurama ili waje kuona miili hiyo. Baada ya kuwasili eneo hilo, mkuu wa kikosi alipiga simu katika kambi kuu ili kutoa ripoti. Wanajeshi walimuita pia mkuu wa tarafa ambaye alituma afisa wa polisi wa uchunguzi na mkuu wa kijiji cha Cibitoke akiambatana na Imbonerakure ( wajumbe wa tawi la vijana la chama cha CNDD-FDD)” alieleza shahidi mmoja.

Wanaume hao waliouwawa kwa kunyongwa kulingana na taarifa za jeshi.

Wakaazi wa eneo hilo la tukio walijawa na hasira baada kuona uhalifu huo.

” Hatuelewi kwa nini miili ya watu waliouwawa hutupwa katika eneo hilo”, analaani mkaazi wa eneo hilo.

Kwa mjibu wake, uchunguzi huru unatakiwa kufanyika ili kufahamu mazingira ya mauwaji ya watu hao wanaopatikana wakiwa maiti katika eneo.

Mkuu wa kijiji cha Cibitoke na afisa wa polisi waliamuru vijana Imbonerakure kuchimba shimu kwa ajili ya kufanya mazishi ya watu hao katika maeneo hayo ambako miili hiyo ilipatikana.

” Nimepata amri kutoka kwa kiongozi wangu ya kuzika watu hao ili wakaazi wasiambukizwi na maradhi”, alifahamisha mkuu wa kijiji cha Cibitoke.

Anafahamisha kuwa maiti 6 zilipatikana katika kijiji hicho mwaka jana. Utambulisho wao bado kujulikana.

Akiulizwa juu ya mkasa huo, mkuu wa tarafa anathibitisha taarifa hizo na kuzidi kuwa utambulisho wa maiti hizo bado kujulikana. Gilbert Manirakiza anasema uchunguzi unaendelea.

Katika kipindi cha miezi miwili, SOS Médias Burundi ilihesabu miili 19 iliyopatikana katika tarafa za Rugombo na Buganda. Kumi na tano mingine iligunduliwa katika tarafa ya Rugombo huku nne mingine ikipatikana tarafani Buganda.

Katika miaka miwili iliyopita, Karibu maiti 200 zilipatikana mkoani Cibitoke, idadi kubwa zikiwa zilipatikana karibu mto wa Rusizi unaotofautisha nchi za Burundi na RDC. Kwa jumla walizikwa bila kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi. Katika matukio machache, vijana wa tawi la vijana wafuasi wa chama cha CNDD-FDD walihukumiwa kwa kosa ” mauwaji na matumizi mabaya ya utawala”.

Watetezi wa haki za binadamu wanaomba viongozi wa Burundi hususan waziri mkuu Gervais Ndirakobuca, mwenye asili ya mkoa wa Cibitoke ” kutumia ushawishi wake ili uchunguzi huru ufanyike na mwanga upatikane kuhusiana na upatikanaji wa maiti hizo.

Previous Bijombo: wapiganaji wa kundi la Twirwaneho wamewauwa wanajeshi watatu wa FARDC
Next Goma: journalists arrested in full coverage of a demonstration against the forces of the EAC